Monday, 10 November 2014

MORANI WAGOMA KABURI KUFUKULIWA.

Morani wenye silaha za adi... yaanimarungu, sime na fimbo wakiandamana kuzuia Mahakama kufukua kaburi.
Wananchi zaidi ya 3,000 wakiwemo Morani waliokuwa na silaha za jadi kama marungu, sime na fimbo katika Kijiji cha Kiushin wilayani Arumeru wamejikusanya kukabili amri ya Mahakama ya Ardhi na Nyumba ya kutaka kufukuliwa kwa kuburi alilozikwa mkazi mwenzao wa eneo hilo...

Aidha, wananchi hao walifanikiwa kuzima jaribio la askari polisi zaidi ya 20 wenye silaha za moto waliokuwa wameongozana na Kampuni ya Udalali ya Nolage ya jijini hapa iliyoidhinishwa na mahakama kuja kufukua maiti hiyo na kuhamisha kaburi.
Wakizungumza kwa jazba wakiwa wamejikusanya katika kaburi hilo, morani hao walieleza kuwa hawapo tayari kuona mwili wa marehemu bibi yao waliyemzika siku chache zilizopita ukifukuliwa kwa amri ya mahakama na kuitaka mahakama hiyo chini ya Hakimu Dorice Mungure ijipange upya dhidi ya hukumu hiyo la sivyo kutatokea maafa makubwa.
“Tumesema kama kaburi tutakuta limefukuliwa ujue kuwa aliyesababisha yote haya atazikwa yeye na familia yake, sisi mila zetu haziruhusu kuzika mara mbili, tutalinda usiku na mchana kaburi hili,’’ alisema mmoja wa wananchi hao, Loselian Solomon.
Awali mahakama hiyo ilitoa zuio la kutofanyika mazishi katika shamba hilo lenye mgogoro baina ya mume wa marehemu, mzee Kuresoi Loilole na mlalamikaji Francis Levava.Hata hivyo, ilielezwa kuwa kabla ya kutolewa kwa ‘order’ ya mahakama, saa 9 alasiri tayari mwili wa marehemu ulikuwa umezikwa saa 8 mchana siku hiyo, Septemba 15 mwaka huu.

Mmoja wa Morani hao akiwa mbele ya kaburi wanalozuia lisifukuliwe.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ya Arumeru, kufuatia kesi ya madai namba 222 ya mwaka 2006 iliyofunguliwa na mlalamikaji, Francis Levava Kivuyo (32), aliyeitaka mahakama hiyo kutoa  uamuzi wa maiti kufukuliwa kutoka shamba hilo ili aweze kuliendeleza.
Mlalamikaji alidaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo  mwaka 1987 alikodisha shamba hilo la mdaiwa Kuresoi Loilole, (70) kwa kiasi cha shilingi 130,000 kwa makubaliano ya kurejeshewa fedha hizo.
Hata hivyo, mwaka 1991 mzee Kuresoi alifanikiwa kupata kiasi hicho cha fedha na kuamua kumrejeshea lakini katika hali isiyo yakawaida mlalamikaji alizikataa fedha hizo na kudai kuwa alishamuuzia shamba hilo.
Ndipo mzee Kuresoi alipofikia hatua ya kufungua kesi Baraza la Ardhi na Nyumba la Kijiji lililompa ushindi mzee huyo  kwa kuamuru shamba hilo arejeshewe.Hata hivyo, Francis aliamua kufungua kesi katika Mahakama ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.
Wakati kesi hiyo ikiendelea, mlalamikaji aliiomba mahakama hiyo isitishe matumizi ya shamba hilo hata hivyo upande wa mdaiwa ulikaidi.

No comments:

Post a Comment