Tuesday, 11 November 2014

MASKINI, WANATAKA KUKATA TENA MGUU WANGU!

Sadick Suleiman akionyesha sehemu ya mguu wake uliokatwa.
Kijana mmoja Sadick Suleiman (24) (pichani),  mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam amesema kuwa madaktari wanataka kuukata mguu wake kwa mara ya tatu baada ya oparesheni mbili kufanyika pasipo mafanikio...

Akizungumza  na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa Hospitali ya Ocean Road, Sadick alisema mguu wake  ulikatwa kwa mara ya kwanza baada ya kuungua moto mwili mzima alipokuwa amekwenda kuvuna korosho.
“Nakumbuka nikiwa darasa  la nne, nikiwa na watoto wenzangu tulikwenda kuokota korosho shambani Mtwara vijijini nilikokuwa nikiishi na wazazi wangu, huko kuna kawaida ya watu kuandaa mashamba yao kwa kuyachoma moto.
“Sasa mimi na mwenzangu ambao tulikuwa wakubwa tukiwa hatujui nini kinachoendelea tulipanda juu  ya mti kwa ajili ya kuangua korosho huku wenzetu wakiwa chini wanasubiri kuokota, tukiwa juu tukaona moto unawaka unakuja tulipokuwa lakini kabla hatujashuka chini, ukatuzingira,” alisema Sadick.
Aliongeza kuwa wenzao waliokuwa chini walifanikiwa kukimbia wao wakiwa juu ya mti, uliwakuta na kila walipojaribu kushuka ndivyo ulivyozidi wakapanda zaidi juu ya mti lakini mwisho walizidiwa na kuamua kujitosa  kwenye moto ambapo yeye aliungua sehemu kubwa ya mwili na mwenzake aliungua mwili mzima ikiwa ni pamoja na kichwani.
Alisema kuwa alifanikiwa kukimbia huku nguo zake zikiwaka moto, alipofika nyumbani kwao  alikuwa tayari ameungua mwili mzima, akakimbizwa Hospitali ya Ndanda, Masasi.Sadick aliongeza kuwa, huko alitibiwa akapona majeraha isipokuwa sehemu ya mguuni kwani mfupa ulikuwa ukionekana ndipo walipokata nyama eneo la paja lake na kuziba ile sehemu.

Mguu wake uliobakia ambao nao unatakiwa kukatwa
“Nilipata nafuu nikaendelea kusoma mpaka kidato cha tatu ambapo tulihamia Mafia na ndugu zangu,  nilikuwa naumwa mara kwa mara lakini nilifanikiwa kumaliza kidato cha nne kwa tabu ndipo nikaanza  kupata vipele ambavyo vilivimba na kuwa vidonda na kunisababishia maumivu makali,” alisema.
Aliongeza kuwa alipozidiwa alipimwa na kuonekana ana kansa hivyo alilazimika kukatwa mguu kwa mara ya kwanza, ilipofika mwezi wa saba alianza tena kuumwa kwa kasi ya ajabu akakatwa kwa mara ya pili sehemu ya mguu iliyobaki.
Baada ya kuendelea kuumwa madaktari wakampa  rufaa  ya kwenda Hospitali ya Muhimbili ambao nao walimpeleka Hospitali ya Ocean Road anakoendelea kutibiwa.“Baada ya kufika Hospitali ya Ocean Road nilianza tiba ya kuchomwa  mionzi lakini bado siwezi kulala wala kukaa naumwa mpaka naona dunia chungu,”  alisema kijana huyo.
Kijana huyo amewaomba Watanzania wenye moyo wa huruma wamsaidie gharama za matibabu kwani  zinahitajika shilingi 1, 470,000. “Fedha hizo ni kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya For Life iliyopo jijini Dar es Salaam ambao wamesema wanaweza kunitibu na kupona tatizo langu,” alisema Sadick.
Yeyote aliyeguswa na tatizo la kijana huyu awasaliane naye kwa simu namba, 0654 003 611 au 0785745261.

No comments:

Post a Comment