
Dar es Salaam. Hatimaye Simba imepata furaha
baada ya jana kuibuka na ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara
msimu huu kwa kuichapa Ruvu Shooting Stars bao 1-0 katika mechi
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam...
Simba ilishuka uwanjani hapo ikiwa na sare sita
katika michezo yao sita ya Ligi Kuu iliyocheza msimu huu na ushindi kwao
ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hiyo.
Katika mechi ya jana, bao la Emmanuel Okwi la
dakika ya 78 lilitosha kuipa ushindi muhimu Simba ambayo hivi sasa
imefikisha pointi tisa kutokana na michezo saba waliyocheza.
Simba ilianza vizuri katika mchezo huo na
kutengeneza nafasi kadhaa kipindi cha kwanza kupitia kwa Okwi, ambaye
shuti lake lilipaa akiwa ndani ya eneo la hatari pamoja na Amissi Tambwe
aliyepiga shuti dhaifu ndani ya hatua sita.
Muda mwingi wa mchezo Simba ilionekana kuhitaji
zaidi ushindi kuliko Ruvu Shooting ambao walitumia zaidi utundu wa
kupoteza muda na kucheza kwa kushambulia kwa kushtukiza.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa suluhu huku
timu zote zikicheza soka la kiwango cha chini. Kipindi cha pili Okwi,
ambaye aliamua kujitoa zaidi katika mchezo huo, alipoteza nafasi ya wazi
alipounganisha vibaya mpira uliodondoka nyuma ya mabeki ukitokea wingi
ya kulia.
Ukidhaniwa kwamba mpira huo utazaa bao la kuongoza
kwa Simba, Okwi aliuunganisha kwa uhakika katika kona ya mwisho ya
lango akidhani utakwenda wavuni, lakini ulitoka nje ya nguzo.
Okwi aliyekuwa msumbufu zaidi katika mchezo huo
pamoja na Ramadhani Singano, angeweza kupata penalti baada ya kuonekana
kama aliangushwa ndani ya eneo la hatari, lakini mwamuzi alisisitiza
kuwa alikuwa bado hajaingia na mkwaju wake wa adhabu kudakwa kirahisi na
kipa wa Ruvu Shooting, Abdallah Rashid.
Hata hivyo, dakika ya 78, kazi nzuri aliyoianzisha
Okwi baada ya kukokota mpira katikati ya mabeki aliimalizia kwa kufunga
bao muhimu kwa Simba baada ya shuti la Elius Maguli kupanguliwa na kipa
wa Ruvu na hivyo Okwi kuumalizia kirahisi.
Ruvu waliamka baada ya kufungwa bao hilo licha ya mwanzo kuonekana wanahitaji suluhu, lakini umaliziaji wao haukuwa mzuri.
Kwa matokeo hayo, Simba sasa imesogea hadi nafasi
ya sita ikiwa sawa na Kagera Sugar yenye pointi tisa pia, lakini ina
uwiano mzuri wa mabao. Kabla ya mchezo wa jana, Simba walikuwa katika
nafasi ya 11.
Akizungumza baada ya mechi, kocha wa Simba,
Patrick Phiri alisema, “Ushirikiano mzuri kati ya Maguli, Tambwe na Okwi
uliisaidia timu yangu kupata ushindi kwa hiyo najisikia furaha.”
No comments:
Post a Comment