Kipa wa Yanga, Juma.....
Kaseja.
SAKATA la
kipa wa Yanga, Juma Kaseja na klabu yake limechukua sura mpya baada ya
uongozi wa Yanga kutoa kauli kali juu ya aliyejitambulisha kuwa ni
meneja wa kipa huyo, huku ikielezwa kuwa kipa huyo amepata ofa ya
kucheza soka Uarabuni.
Abdulfatah Saleh ambaye amejitambulisha kuwa ni meneja wa mchezaji
huyo, amenukuliwa na vyombo vya habari likiwemo gazeti hili, akisema
kuwa Yanga imevunja mkataba na mteja wake kutokana na kukiuka masharti
ya mkataba.
Akijibu madai hayo, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, ameliambia
Championi Ijumaa kuwa, kisheria wao hawamtambui huyo anayejiita meneja
wa Kaseja na hivyo hawawezi kutambua madai ya kuvunjwa kwa mkataba kama
inavyoelezwa.
Njovu alikataa kujibu swali la mkataba huo kwa njia ya simu na kuomba
atumiwe barua pepe, alipoulizwa kupitia barua pepe, alijibu kwa kifupi
kama ifuatavyo:“Siwezi kukujibu maana mchezaji Juma Kaseja hana meneja
anayetambulika na taasisi yoyote, iwe Yanga, TFF au hata Fifa.”
Kisha baada ya hapo akaambatanisha na majina ya mawakala ambao
wanatambulika Fifa, akiwataja kuwa ni Ahmed Binkleb, John Ndumbaro,
Mehdi Remtulla na Ally Saleh.
Wakati hayo yakiendelea, Abdulfatah Saleh ameliambia gazeti hili kuwa
Kaseja anaendelea kupata ofa mbalimbali ikiwemo kutoka klabu mbili za
Dubai.
“Kaseja kubaki Yanga baada ya mzunguko huu wa sasa ni mgumu kutokana
na Yanga kukiuka masharti ya mkataba kwa kushindwa kumalizia fedha za
usajili zilizobaki, shilingi milioni 20, ambazo zilitakiwa zilipwe kabla
ya Januari 15, mwaka huu,” alisema Abdulfatah.
No comments:
Post a Comment