Wednesday, 29 October 2014

HANS POP APIGWA STOP SIMBA!

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope.

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope pamoja na wajumbe wengine wa kamati za klabu hiyo, wamepigwa marufuku na uongozi kuzungumzia klabu hiyo kwani ni nje ya mamlaka yao na nyadhifa zao.
Hans Pope amekuwa akizungumza katika redio na TV, pia kunukuliwa na magazeti mara kwa mara juu ya mwenendo wa timu ya Simba huku akiyazungumzia mambo ya kiuongozi na ya kiutaalam zaidi.Mbali na yeye, pia viongozi wengine wa Simba wamekuwa wakizungumza mara kwa mara kuhusu timu hiyo.
Katibu wa Simba, Stephen Ally alisema kuwa kamati ya utendaji ya klabu ilikaa kikao juzi na kuamua kuwa siyo kila kiongozi ataruhusiwa kuzungumzia mambo ya klabu bali kamati iliamua jukumu hilo kufanyika na viongozi wanne tu.
Viongozi wenye mamlaka ya kuizungumzia klabu ni rais, makamu wa rais, katibu na msemaji wa klabu. Kiongozi mwingine nje ya hao hatakuwa na mamlaka ya kuifanya kazi hiyo.
Stephen aliongeza, japokuwa Hans Pope amezoeleka katika vyombo vya habari, tayari wamemtumia taarifa ya kuacha kufanya hivyo na kama atazungumza basi yawe ni masuala yake binafsi na siyo yahusuyo timu au klabu kwa jumla.
“Wenye mamlaka ya kuizungumzia klabu kwa ujumla ni watu wanne tu na siyo kila mwenye cheo Simba ana uwezo wa kutoa kauli juu ya klabu na ikanukuliwa na wanahabari.Hans Pope tumeshamueleza, mara baada ya kikao alipewa taarif kuwa hatakiwi kuzungumza kuhusu timu tena.,” alisema Ally.
Hans Pope ni kiongozi wa muda mrefu sana Simba na alikuwa kwenye timu hiyo tangu utawala wa aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo, Ismail Aden Rage.
Haya yametokea baada ya hivi karibuni wachezaji watatu wa Simba, Amri Kiemba, Haroun Chanongo na Shaban Kisiga kusimamishwa kutokana na utovu wa nidhamu na kiwango kibovu, ambapo viongozi mbalimbali wamezungumzia suala hilo, jambo ambalo limezua maswali mengi.

No comments:

Post a Comment