Msanii wa Hip Hop, Rashid Makwiro 'Chid Benz' akiwa chini ya ulinzi akipelekwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu leo.
MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Rashidi Makwiro ‘Chid Benz’, jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salam na kusomewa mashtaka matatu yanayomkabili....
Oktoba 24, mwaka huu, Chid Benz alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akiwa na dawa za kulevya wakati akikaguliwa kabla ya kwenda jijini Mbeya kwa ajili ya kutumbuiza.
Akisoma mashtaka mahakamani hapo jana mbele ya hakimu,
Waliarwande Lema, mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, Mwanaamina Komba, alisema kuwa Oktoba 24, mwaka huu, Chid Benz alikamatwa akiwa na dawa hizo ambazo ni heroine gram 0.85 zenye thamani ya Sh 38,638, bangi zenye thamani ya Sh 1,720 pamoja na vifaa vya utumiaji wa kuvuta dawa hizo ambavyo ni kifuu pamoja na kijiko.
Hata hivyo, mwendesha mashtaka huyo, alisema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea. Chid alikanusha kukutwa na madawa hayo.
Naye hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alisema kuwa kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa ana haki ya kupata dhamana ambapo anatakiwa kutoa kiasi cha Sh 1,000,000 (milioni moja) pamoja na wadhamini wawili wasiokuwa na hatia.
Hata hivyo, Chid Benz alishindwa kutimiza masharti hayo, hivyo kurudishwa rumande hadi hapo atakapokuwa ametimiza masharti hayo.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Novemba 11, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment