Wednesday, 31 December 2014

HAYA NDIYO MALENGO YANGU 2015, WEWE JE?

Kwanza nawatakieni tena wote heri ya mwaka mpya 2015, hata wale walioanza mwaka kwa ‘kuwekwa kiporo’, waliofukuzwa kazi na bosi, waliogawana ule mkwanja....

waliokosa ule mkwanja, wanaolalamika kwa kuwa walikosa ule mkwanja, wanaolalamika kwa kuwa wanaona wananchi waliukosa ule mkwanja, wanaolalamika kuhusu ule mkwanja kusudi wapate mkwanja, wanaolalamika kwa nini watu wanalalamika kuhusu ule mkwanja,
wanaolalamika kuwa watu wasilalamike kuhusu ule mkwanja, na Taifa lote kwa jumla, bila kuniacha mimi mwenyewe au vipi?
Kila unapoanza mwaka lazima upime yaliyopita na ujipange kwa yajayo. Mimi pia nimeamua nijiwekee mikakati ya 2015.
Lazima 2015 nipunguze kitambi. Wiki hii nimeshachelewa lakini kuanzia wiki ijayo ntakuwa naamka kila siku saa kumi na moja naanza jogging na mazoezi ya kuruka kichurachura kuzunguka uwanja wa mpira hapo mtaa wa pili, mwaka huu sitanii lazima kitambi kiende.
Lazima 2015 nihakikishe kila mwezi naweka benki elfu 50. Yaani sitaki mchezo hii habari ya kufikia Januari nahaha kutafuta ada ya shule ya watoto, huku mama mwenye nyumba kanikalia kooni kama miye siyo mtoto wa mwanamke mwenzie lazima iishe, yaani hata kama nikipata mchepuko mpya nakomaa nauambia laiv ‘Mi sina pesa’. Au ukiomba vocha najibu ‘Mi siyo wakala’  Kikubwa ni kula jiwe.
Lazima 2015 nioe demu wa Bongo Muvi. Kwani wengine wana nini? Ujue watu huwa wanakosea sana, wanadhani eti hela ndiyo itasaidia, hapana hawa wadada ni binadamu kama sisi, hivyo ukimlilia hali na kumwambia huna hela lakini unampenda atakuelewa tu. Maisha ya ndoa muhimu mapenzi. Na wengi wameshasema wanatafuta watu wa kuwazalisha, mimi ni dume la mbegu, ulizia kijijini kwetu usikie sifa za ukoo wetu.
Kila mtu ana watoto nane au tisa. Kwa hiyo mwaka huu ndugu zangu tegemeeni ndoa yangu na supastaa, nipeni wiki mbili nijue yupi nimuibukie. Nitatumia staili ya ana ana ana doo, kachanika pasto, isplingi matingoo, kumchagua anayefaa.
Usafiri 2015 lazima. Sina makuu hata kagari hata kadogo tu kama hutu tuvitz katanitosha, unajua ukoo wetu hakuna aliyewahi kuwa na gari lake, unajua jinsi Waafrika tulivyo na roho mbaya unaweza kukuta kuna kazee pale kijijini kaliloga ukoo wetu tusipate gari, ntajitahidi kuhudhuria kwa yule Mzee anayeonekanaga kwenye TV anahubiri halafu watu wanamtunza kama muimba taarab, nasikia ukienda kule mara mbili tatu mikosi yote inayeyuka unapata Kivitz chako kiulaini.
2015 cheo lazima. Nilichelewa kugombea uenyekiti serikali za mtaa maana, nilipotaka kujiunga na chama hiki wapambe wakaniambia huko utashindwa, nikataka kwenda chama kile wakaniambia huko ndiko kabisa hakuna mvuto utashindwa, nikachelewa kujiandikisha, sasa najipa muda mpaka mwezi wa nne ntakuwa nimepima maji chama gani kitashinda basi najitosa huko kugombea Ubunge. Ndugu zangu niombeeni, nikipata Ubunge matatizo yetu yote yameisha, si mnajua mimi ni matirio kabisa ya kuweza kuwa Waziri, tukifika Uwaziri hapo ni funga kazi.
2015 lazima nitoe singo. Kwani mimi nina nini na Diamond ana nini? Nikitoa Singo moja tu hayo yote hapo juu nimesovu. Kasoro lile la kitambi lakini ukiwa na singo unatengeneza kundi la madensa unafanya nao mazoezi mpaka kitambi chote kinayeyuka si ndiyo. Singo iki-hiti, Ubunge unakuwa rahisi kabisa, wananchi wanapenda sana wasanii.
Mwaka huu pombe basi. Nitajitahidi ingawaje kimsingi bado sijaona sababu kwa nini niache pombe, kwa mwaka huu mara mbili tu ndiyo nimeangusha gari baa. Sasa  mtu nakunywa kila siku mwaka mzima halafu bahati mbaya mara mbili tu nimeangusha gari, siyo mbaya maana kuna watu wanaangusha deile. Kwa hiyo tuseme ntapunguza pombe.

No comments:

Post a Comment