Yawezekana wewe ni mwanaume au mwanamke ambaye unafanya kazi na
umpendaye, awe ni mke, mchumba au mpenzi. Je,..
kuna faida gani
unazozipata kutokana na kufanya kazi ofisi moja na umpendaye? Vipi
kuhusu hasara na changamoto?
Bila kujali kama mmekutana sehemu ya kazi na kuanzisha uhusiano wa
kimapenzi au mlianza kabla lakini baadaye mkajikuta mkifanya kazi sehemu
moja, lazima ujue kwamba zipo faida lakini kama hiyo haitoshi, zipo
changamoto nyingi ambazo ni lazima ujue namna ya kuzishughulikia ili
kuwa na uhusiano bora wa kimapenzi na amani ya nafsi yako.
FAIDA KUBWA
Faida kubwa ya kufanya kazi pamoja ni kwamba unapata
muda wa kutosha wa kuwa karibu na mwenzi wako. Kwa wale ambao wana hulka
ya wivu au wanashindwa kuwaamini wenzi wao, kufanya kazi pamoja
huwasaidia kutulia kwa sababu watakuwa na uhakika na mahali walipo au
shughuli wanayoifanya wenzi wao kwa sababu wanawaona na wanashinda nao
siku nzima.
CHANGAMOTO ZAKE
Changamoto za kufanya kazi ofisi moja na
umpendaye, huwa ni nyingi kuliko faida na usipokuwa makini zinaweza
kusababisha kuyumba, kulegalega au kuvunjika kabisa kwa uhusiano wako wa
kimapenzi na umpendaye.
Changamoto ya kwanza na kubwa huwa ni kushindwa kutenganisha mambo ya
nyumbani na mambo ya kazini. Kama jana usiku mlikorofishana na mwenzi
wako, uwezekano mkubwa ni kwamba chuki za nyumbani utazileta kazini na
matokeo yake, ufanisi wa kazi utapungua.

Pia, kihulka binadamu ameumbwa kuwa na muda wa kukutana na watu
wengine, kubadilishana mawazo na kuingiza vitu vipya kichwani. Sasa
inapotokea wewe na mwenzi wako mnafanya kazi pamoja, ni kwamba mtajikuta
muda mwingi mkiutumia pamoja na kushindwa kuchanganyika na watu
wengine, jambo ambalo kitaalamu husababisha msongo wa mawazo.
Changamoto nyingine, ni pale inapotokea mmoja kati yenu ameharibu
kazi. Kwa kawaida, mabosi huwa wakali inapotokea mfanyakazi amefanya
kosa lililosababisha hasara, iwe ni kwa bahati mbaya au makusudi.
Mabosi wengine hufikia hatua ya kuwafokea au kuwaadhibu waliofanya
uzembe huo. Utajisikiaje mwenzi wako anapoadhibiwa mbele yako kwa sababu
amefanya makosa kazini?
Vipi kuhusu mwenzi wako anapokorofishana na wafanyakazi wenzake?
Wahenga walisema vikombe vinapokaa kabatini pamoja, havitakosa
kugongana. Hivyo mwenzi wako anapofanya kazi, ni lazima itatokea
akakorofishana na wafanyakazi wenzake.
Je, utajisikiaje kusikia mwenzi wako akitukanana au kupandishiana na
mtu mwingine kwa sababu ya kazi? Kimsingi utaambulia ‘stress’ za kutosha
ambazo huenda zikapunguza ufanisi wako wa kazi.
NINI CHA KUFANYA?
Licha ya changamoto nilizozieleza hapo juu,
wapo wapendanao wengi ambao huweza kudumu na kuishi maisha ya furaha
japokuwa wanafanya kazi ofisi moja. Hata wewe unaweza kuwa na uhusiano
bora licha ya kuwa unafanya kazi ofisi moja na mwenzi wako endapo
utazingatia mambo ya msingi ambayo nitakufafanulia kwa kina kwenye
sehemu ya pili ya makala haya.
Usikose wiki ijayo ambapo tutaangalia kwa kina mbinu za kupambana na
matatizo yanayotokea kazini kwa sababu ya kufanya kazi ofisi moja na
mwenzi wako.
No comments:
Post a Comment