
Wachezaji wa Simba wakifanya mazoezi kwenye ufukwe wa coco kujiandaa na mechi dhidi ya Ruvu Shooting Dar es salaam...
Dar es Salaam. Ni presha kila kona Simba.
Ndivyo unavyoweza kusema wakati kamati ya utendaji ya klabu hiyo
ikikutana leo, kocha Patrick Phiri ameanza upya kuwanoa wachezaji kwa
kuwapeleka ufukweni ili kujenga stamina.
Dharura hiyo ya kikao cha kamati ya utendaji
inaonyesha hali si shwari ndani ya Simba, jambo linalowafanya viongozi
wahangaike ili kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.
Kwa upande wao, viongozi wanawatuhumu baadhi ya
wachezaji kucheza chini ya kiwango, utovu wa nidhamu huku kocha Patrick
Phiri akipewa mtihani wa mechi ili akishindwa, iwe sababu ya kutimuliwa.
Mashabiki wengi wa klabu hiyo wanaamini kuwa kocha
anaonewa, tatizo lipo kwa uongozi unaotakiwa kujichunguza ili kuona
wapi umekosea na kuondoa kasoro zilizopo na si kukimbilia kumlaumu
kocha.
Rais wa Simba ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya
utendaji, Evance Aveva alisema jana kuwa kamati yake inakutana leo
kujadili mwenendo mbovu wa timu pamoja na suala la kocha na wachezaji
waliosimamishwa.
Wachezaji waliosimamishwa, Amri Kiemba, Shaaban Kisiga na Haroun Chanongo, wanadaiwa pia kuhusika na utovu wa nidhamu.
“Kamati ya Utendaji itakutana Jumatano (leo) ili
kuamua hatima ya wachezaji na kesho tutatoa majibu, waendelee na adhabu
au la,” alisema Aveva.
Kuhusu mwenendo wa sare za timu hiyo msimu huu,
Aveva alisema hiyo ni sehemu ya mchezo na klabu yake siyo ya kwanza
kupata matokeo hayo, ijapokuwa si mazuri, wala si mabaya.
Pamoja na Aveva kukubali matokeo, uongozi wake
umempa Phiri mechi mbili akiwa amebakiza moja dhidi ya Ruvu Shooting
Jumamosi ili kunusuru kibarua chake.
Baada ya sare na Mtibwa Sugar, Jumamosi iliyopita,
Phiri ameamua kuwarudisha mazoeni wachezaji wake, safari hii ufukweni
ili kuwaongezea stamina.
Alisema kikosi chake kinacheza vizuri kwa muda
mfupi, kadri muda unavyokwenda, kipindi cha pili wachezaji huchoka,
kuwaruhusu wapinzani kutawala na kusawazisha mabao.
“Nimeona kuna tatizo la kukosa stamina, jambo
ambalo limekuwa likitugharimu, kipindi cha pili, kwani mara nyingi sisi
huanza kufunga, lakini mabao yanarudi, hicho si kitu kizuri.
No comments:
Post a Comment