Monday, 3 November 2014

NINI CHA KUFANYA WAZAZI, NDUGU WANAPOMCHUKIA UMPENDAYE?


Tuliangalia mfano wa jinsi mwanaume mmoja ambaye yupo ndani ya ndoa kwa kipindi cha miaka kumi, alivyokuwa kwenye mgogoro mkubwa baada ya mke wake wa ndoa kutokea kuwachukia na kuwadharau mno wazazi wa mwanaume kwa sababu ambazo anazijua mwenyewe.
Wazazi nao wakaja juu na kumwambia achague moja, mke au wazazi na kujikuta akishindwa kuamua. Leo tunaendelea kueleza nini cha kufanya unapotokewa na hali kama iliyomkuta ndugu yetu huyo.
NINI CHA KUFANYA?
1. TAFUTA CHANZO CHA TATIZO
Kama nilivyoeleza wiki iliyopita, hatua ya kwanza unayotakiwa kuifanya, ni kutafuta chanzo cha tatizo. Kwa nini mke/mume awachukie wazazi wako? Na kwa nini pia wazazi au ndugu wamchukie mume/mke wako? Lazima kuna sababu kwani hakuna chuki ambayo huwa haina chanzo.
Ukichunguza utagundua kuwa kuna jambo lililosababisha hayo yote, huenda ni kwa sababu wazazi wako walikuwa wanampenda mtu mwingine uliyewahi kuwa naye kwenye uhusiano wa kimapenzi. Au pengine mwenzi wako anawatuhumu wazazi wako kwamba wanashirikiana na wewe kuandaa njama za kumuondoa ili aje mtu mwingine au kuna tuhuma za ushirikina kati ya pande hizo mbili.
Ukishakijua chanzo, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutatua tatizo.
2. ZUNGUMZA NA KILA UPANDE
Baada ya kukijua chanzo, anza kuzungumza na mwenzi wako, mueleze jinsi unavyojisikia vibaya kutokana na uhasama uliopo kati yake na wazazi wako. Tumia lugha ya upole na muulize anataka nini kifanyike ili chuki yake iishe.
Kama anataka umuoneshe upendo wa dhati, nadhani hilo litakuwa ndani ya uwezo wako, muahidi kwamba kama wewe ndiyo chanzo, utabadilika kwa lengo la kumaliza matatizo. Hata ikibidi, mpe zawadi ambazo zitamfurahisha na kumfanya alegeze msimamo wake.
Baada ya hapo, hamia upande wa pili, zungumza na wazazi wako kwa heshima na uwaeleze jinsi unavyoumia kutokana na matatizo yanayoendelea kati yao na mwenzi wako. Kamwe usioneshe dharau kwao, zungumza nao kwa adabu huku ukiwapa heshima zote wanazostahili kisha waulize wanataka nini kifanyike ili uhasama uishe.
Kama wanataka mwenzi wako akawaombe msamaha, waahidi kwamba utasimamia hilo hadi litimie ila kama wanataka muachane, nadhani huo hautakuwa uamuzi sahihi, endelea kuzungumza nao mpaka muafaka upatikane.
3. WAPATANISHE
Baada ya kuwa umeshazungumza na pande zote mbili, andaa muda maalum ambao utawakutanisha wote, kama inawezekana unaweza pia kuwaita baadhi ya watu wachache unaowaamini kama washenga au viongozi wa dini waliofungisha ndoa yenu kisha kila mmoja azungumze dukuduku lake na mwisho, anayestahili kuomba radhi afanye hivyo.
Mpaka hapo tayari utakuwa umefanikisha kupatikana kwa suluhu, busara kubwa itumike kuwapatanisha ili mkimaliza kikao hicho cha suluhu, asiwepo ambaye bado atakuwa na dukuduku.
Baada ya kupatikana kwa suluhu, kuwa makini ili yale yaliyosababisha matatizo awali, yasijirudie tena.
Angalizo: Ni rahisi kumdhibiti mwenzi wako akafanya vile unavyotaka kwa lengo la kupata suluhu kuliko wazazi wako hivyo unatakiwa kuelekeza nguvu zako kwa mwenzi wako zaidi huku ukiepuka kuwakosea adabu wazazi wako. Usioneshe kuegamia upande wowote.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.

No comments:

Post a Comment