Tuesday, 11 November 2014

KAKOBE - 6.

Askofu Kakobe
Naendelea kuwaletea mahojiano kati yangu na Askofu Kakobe kuhusiana na maisha yake ya wokovu.
Divai aliyoitengeneza Yesu ni karibu mapipa saba!...

Divai hii haikuwa kileo au pombe maana aliudhihirisha utukufu wake. Ingekuwa amewapa watu kileo, ingekuwa aibu kwake badala ya utukufu.  Ilikuwa ni divai mpya au divai tamu yaani juisi ya zabibu, tofauti na divai iliyochanganyika au kuchachuka ambayo ni pombe angalia Mithali  9:4-6; 23:29-30; Yoeli 3:17-18).  Hatupaswi kunywa mvinyo au divai iliyochanganyika ambayo ni kileo.
Mwandishi: Kuna baadhi ya watu huwa wanasema wamewahi kukutana au kumuona Mungu, je, inawezekana watu kumuona Mungu hapa duniani?
Askofu Kakobe: Mtu hawezi kumuona Mungu ambaye ni roho kwa macho ya kimwili, akaishi, kwa macho ya kimwili, mtu anaweza kumuona Mungu kwa sehemu tu ya umbo na siyo uso angalia Hesabu 12:8; au Kutoka 33:17-23. Hata hivyo, mtu anaweza kumuona Mungu anapokuwa katika roho, kwa macho ya rohoni.
Mahali popote mtu alipomuona Mungu, alimuona katika hali hii, macho ya mwili na mwili wote ukiwa hauna sehemu katika jambo hili angalia Ufunuo 1:9-10; 2 au Wakorintho 12:1-4; au Matendo7:56. Katika roho, mtu ndipo pia anaweza kusema na Mungu uso kwa uso kama rafiki yake kama ilivyoandikwa katika Kutoka 33:11. Tunalojifunza hapa ni kwamba, Musa na watu wengine waliomuona Mungu kwa macho ya rohoni, walifanya hivyo kwa muda kidogo tu na wakarudia macho ya mwilini.
Mwandishi: Watu wengi sana wamezungumzia Jehanam, hebu tufafanulie, huko ni wapi na kukoje kwa mujibu wa ulivyosoma?
Askofu Kakobe: Mwanangu, huko kunatisha, nashindwa hata nikueleze vipi unielewe. Kuna moto wa milele, hatukuwekewa wanadamu bali shetani soma Mathayo 25:41. Kama utakwenda huko baada ya kusoma “note” hii, itakuwa ni kwa sababu ya kiburi chako tu na kushupaza shingo yako na kukataa kulitendea kazi Neno hili.  Moto wa Jehanam siyo mahali pa mchezo kama walimu wa uongo wanavyofundisha. 
Mwandishi: Wapo watu wanaosema kuwa Jehanamu watu wakitupwa huko, wataungua kisha kuteketea kabisa, unasemaje kuhusu hilo?
Askofu Kakobe: Kwa ujumla, mafundisho yote haya yanatokana na shetani, yanalenga kuwafanya watu waendelee kutenda dhambi, huku wakipuuza ukweli juu ya Jehanam, kwa kuwaza kwamba watateseka dakika chache na kupotea kabisa na ndiyo mwisho. Jehanum ya moto, au kuzimu, ni shimo kubwa na refu sana lililojaa moto. Moto wa Jehanam huchochewa mfululizo, ili usizimike; lakini huchochewa na pumzi ya Bwana, yaani pumzi maalum ya Mungu mwenyewe soma Isaya14:15.
Mwandishi: Maandiko yanasemaje kuhusu Jehanamu?
Askofu Kakobe: Maandiko yanasema ukali wa moto wa Jehanam, unatisha angalia Waebrania 10:26-27. Moto wa Jehanam ni tofauti kabisa; Ni moto wa rangi nyeusi, unaosababisha giza na kumfanya mtu aliye motoni, awaone wenzake wachache tu wa karibu naye, hivyo hamna faraja ya kusema “tuko wengi!” Moto huu mweusi, ndiyo maana unaitwa “giza la nje” angalia Mathayo 8:11-12 . Walioko huko motoni, wakimuona yeyote mwingine kutoka duniani, ambaye alikuwa na nafasi ya kusikia habari kama hizi na akazipuuza, kisha akawafuata huko motoni, humwambia, “Je, wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi!” (soma Isaya 14: 10).
Mwandishi: Kuna hili suala la Tanganyika kutaka kurejeshwa, limesemwa katika Rasimu ya Katiba iliyotengenezwa na Tume ya Warioba, wewe unasemaje kuhusu suala hilo? Askofu Kakobe: Inachekesha sana, huku kwetu (Tanganyika) ni nchi gani? Kwa  nini tukubali Zanzibar nchi na huku kwetu ni nini?
Wanasema kuna mambo ya muungano na mambo yasiyo ya muungano, wanasema kuna mambo yasiyo ya muungano yanashughulikiwa na Zanzibar na mambo ya muungano yanashughulikiwa na nani na nchi gani?  Haiko, imeyeyuka hewani ikapotelea na Nyerere kwa sababu siyo mpango wa Mungu ndiyo maana miaka nenda miaka rudi kumekuwa na vikundi vinavyoibuka hata ndani ya uongozi wa serikali kutaka Tanganyika irudishwe.
Utaona tume moja baada ya nyingine, Tume ya Nyalali, Tume ya Kisanga, tume chungu nzima siyo kitu kimeanza na  Jaji (Joseph) Warioba,  ilianza tangu Nyerere mpaka ikaja G 55 wabunge vigogo wa CCM walitaka Tanganyika enzi za Nyerere aliyekuwa anaogopwa kama simba lakini watu walidai Tanganyika. Nyerere ilikuwa shughuli lakini bado akiwa bado anaishi kukatokea watu 55 wakadai Tanganyika kwa sababu ni Mungu anayetaka iwe.
Mwandishi: Wewe unadhani hili la kudai Tanganyika litakuwa mwisho wake Dodoma kwenye Bunge Maalum la Katiba?
Askofi Kakobe: Hapana. Kelele za Tanganyika zitaendelea na hakuna mtu atakayezima. Kila anayepigania Tanganyika ana Mungu ndani yake, ni suala la muda tu, Tanganyika lazima irudi huo ni urithi wa Mungu aliyetuwekea mipaka. Anayeipigania Tanganyika nampongeza kwa sababu Mungu yupo ndani yake.
MWISHO.

No comments:

Post a Comment