Tuesday, 11 November 2014

JIMBO LA MVOMERO TATIZO KUBWA NI MAPIGANO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI..

Mheshimiwa Amos Gabriel Makalla akizungumza jambo.
Mvomero ni miongoni mwa wilaya sita zinazounda Mkoa wa Morogoro, pia ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mheshimiwa Amos Gabriel Makalla (pichani)kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji...

Kwa upande wa Kaskazini, Mvomero inapakana na Mkoa wa Tanga, Kaskazini Mashariki inapakana na Mkoa wa Pwani na Mashariki na Kusini Mashariki kuna wilaya za Morogoro Vijijini na Morogoro Mjini wakati upande wa Magharibi kuna Wilaya ya Kilosa.Uwazi lilifunga safari mpaka kwenye jimbo hilo na kuzungumza na wananchi ambao walieleza matatizo mbalimbali yanayowakabili.
MATATIZO YA WANANCHI
Tatizo kubwa lililoelezwa na wananchi wengi wa jimbo hilo, ni migogoro ya ardhi iliyokithiri ambayo imekuwa ikisababisha mapigano ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji wanaogombea ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji.
Wakulima wanalalamika kwamba wafugaji hasa wa jamii ya Kimasai, wamekuwa wakiingiza mifugo yao kwenye mashamba yao, jambo linalosababisha hasara kubwa na kurudishwa nyuma kimaendeleo.
“Kwa mfano mtu unahangaika kwa kipindi kirefu kulima, kupalilia na kuhakikisha shamba linakuwa katika hali nzuri, halafu Wamasai wanaingiza ng’ombe zao na ndani ya saa chache zinakula kila kitu na kuacha shamba likiwa jeupe, je, ni halali kweli hii?” Isihaka Lihendeko, mkulima wa jimbo hilo alimwambia mwandishi wetu.
“Hawa wakulima ni wakorofi, wanakuja kulima kwenye maeneo yetu ya kulishia mifugo, sisi tukachunge wapi ng’ombe wetu? Halafu ng’ombe wakipita hata kwa bahati mbaya kwenye mashamba yao wanawakata miguu au kuwaua, yaani ni fujo tupu huku, tunaomba serikali itusaidie,” Laizer Ole Saboi, mfugaji wa eneo hilo naye aliliambia Uwazi.
Mbali na tatizo hilo, uhaba wa maji safi na salama ya kunywa ni tatizo lingine lililoelezwa na wananchi wa jimbo hilo. Pia kuna uhaba wa madarasa na vifaa vya kujifunzia, ukosefu wa madawa katika hospitali na miundombinu mibovu, upungufu walimu na maabara kwenye shule za sekondari na za msingi ni matatizo mengine yaliyoainishwa na wananchi wa Mvomero.
MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kuwasikiliza wananchi wa jimbo hilo, Uwazi lilianza kumsaka Mheshimiwa Amos Makalla ambapo alipopatikana, alikuwa na haya ya kueleza:
“Ni kweli kuna matatizo makubwa kati ya wafugaji na wakulima jimboni kwangu lakini najitahidi usiku na mchana kutafuta suluhu ya kudumu. Awali nilikuwa nikitumia serikali ya wilaya kutafuta suluhu lakini ikashindikana.
“Baada ya hapo, niliwasiliana na Waziri Mkuu, Mzengo Pinda na kumuomba anipe mawaziri wa wizara zote zinazohusika kwenye mgogoro huo, wakiwemo Waziri wa Kilimo, Waziri wa Mifugo, Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye kwa kipindi hicho alikuwa ni Nchimbi na Waziri wa Ardhi.
“Tukaenda nao eneo la tukio ambapo walijionea hali halisi na kwa pamoja tukaanza kulishughulikia tatizo hilo. Nashukuru mpaka sasa hali imetulia ingawa bado tatizo limebaki kwa wafugaji ambao wanahamahama ambao kwa kuwa hawajui makubaliano tuliyofikia, wameendelea kutusumbua na kusababisha mapigano ya mara kwa mara.
“Pia nimeanzisha kampeni za kuwakutanisha wakulima na wafugaji ambapo tunapita vijijini na kuwaeleza wananchi umuhimu wa kila mmoja kuheshimu mali za mwenzake, mkulima aheshimu mali za mfugaji na mfugaji naye afanye hivyohivyo.
Kimsingi tatizo limepungua sana tofauti na mwanzo.
“Suala la huduma za kijamii, nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia wananchi wa Mvomero na hivi sasa hali ni tofauti sana na kipindi nilichokuwa naingia madarakani. Nawaomba wananchi wawe na imani na mimi kwani nitahakikisha nazimaliza kero zote zinazowasumbua,” alisema Makalla.

No comments:

Post a Comment