Friday, 31 October 2014

YAFAHAMU MATATIZO KATIKA MFUMO WA UZAZI KWA MWANAMKE

Mfumo wa uzazi wa mwanamke unahusisha viungo vyake vya uzazi vya nje na ndani.........
Viungo vya uzazi vya ndani ni kizazi, mirija na vifuko vya mayai.Mabadiliko mbalimbali hutokea katika mwili wa mwanamke ambayo huhusiana na mfumo wa homoni au vichocheo. Mabadiliko rasmi huanza wakati wa kuvunja ungo.
Baada ya kuvunja ungo mabadiliko yanayotokea ni kuongezeka kwa mwili lakini kwa upande wa akili zinakuwa bado hivyo huonekana msichana mkubwa lakini mtoto.Ukuaji huu wa mwili huwa hauendani na kukomaa kwa viungo vya uzazi.
Msichana huanza kuvunja ungo kuanzia umri wa miaka 12 hadi 14, wapo wanaowahi zaidi, yaani chini ya miaka 12 na wapo wanaochelewa zaidi ya miaka 14.Inaweza pia kutokea mwanamke akaendelea kuwa mtu mzima yaani zaidi ya miaka 18 na asiwe amevunja ungo. Tatizo hili husababishwa na mambo makuu mawili. Kwanza ni kutokamilika kwa viungo vya uzazi ambapo wengine wamezaliwa hivyo, hawana uke au wengine uke umeziba kwa ngozi laini.
Matatizo katika mfumo wa homoni pia husababisha mwanamke asione damu yake na wasichana wa aina hii utaona wamekuwa wakubwa lakini hawana matiti wala vinyweleo kwapani au sehemu za siri ingawa umri wao unazidi miaka 18.
Mabadiliko makuu katika mfumo wa homoni wa mwanamke huanzia katika vifuko vya mayai. Homoni hizi ndizo husimamia ufanyaji kazi wa uzalishaji mayai, mfuko wa uzazi na mfuko wa mirija ya mayai.
Homoni pia humsaidia mwanamke awe na hamu ya tendo la ndoa na kulifurahia, apate siku za hedhi na abebe mimba na kuzaa.

Matatizo katika kizazi
Matatizo katika kizazi yapo mengi lakini tutazungumzia yale makubwa.
Kuna tatizo linaitwa Endometriosis, hapa lile tabaka la ndani la kizazi linaota nje ya kizazi. Mwanamke mwenye tatizo hili husumbuliwa na maumivu ya tumbo chini ya kitovu mara kwa mara, maambukizi ndani ya kizazi pia huchangia.
Mwanamke huweza kukabiliwa na tatizo la uvimbe ndani ya kizazi au Fibroid. Fibroid zinaweza kuwa ndani ya kizazi, katika misuli ya kizazi na nje ya kizazi.Uvimbe wa Fibroid unaweza kuondolewa kwa njia ya dawa kutegemea na ukubwa wa uvimbe. Wapo ambao walikuwa na aina hizi za uvimbe ukatibiwa na ukapona.
Maambukizi ya ndani ya kizazi husababisha mwanamke apate maumivu makali ya tumbo chini ya tumbo, maumivu baada ya tendo la ndoa na kuhisi maumivu ya kitu kinasukumwa ukeni. Tatizo la kizazi huzuia mwanamke asipate mimba.
Matatizo ya mirija
Mirija ya mayai imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Kwanza ni sehemu nyembemba inayoungana na kizazi, sehemu pana katikati ya mirija na sehemu ya mwisho iliyokaa kama vidole au tarumbeta.
Urutubishaji wa yai hufanyika katika mrija na baada ya hapo yai lililorutubishwa husafiri hadi ndani ya kizazi ambapo mimba hukua na kutunzwa.
Mirija ya mayai ni laini sana na ni rahisi kuathirika. Mrija huathirika kwa kupata maambukizi, kuumia kwa kupasuka pale mimba inapotungwa na kukua kwenye mirija, mirija inapata maambukizi toka ndani ya kizazi, maambukizi ya kizazi kuanzia ukeni au ndani ya kizazi chenyewe kama mimba ikiharibika au itatolewa kwa makusudi.
Kuziba kwa mirija husababisha mwanamke kutoshika mimba au kutunga nje ya kizazi, yaani kwenye mrija.
Mirija inapoziba athari zake ni kutopata ujauzito, lakini pia mirija inaweza kuvimba kwa kujaa usaha au maji na kusababisha apate maumivu ya chini ya tumbo yanayosambaa upande wa kulia na kushoto.
Tatizo la mirija kujaa usaha au maji huwa linatibika na pia mirija iliyoziba huweza kutibika kutegemea na uzibaji.Matibabu haya hupatikana kwa madaktari wa kinamama kwenye hospitali ya mikoa na wilaya.

Itaendelea wiki ijayo

No comments:

Post a Comment