Friday, 31 October 2014

ECOWAS YAIONYA BURKINAFASO

Waandamanaji wakipozi wakati wa vurugu za jana nchini Burkina Faso.
Wanajeshi wakijaribu kutuliza vurugu za waandamanaji....
JUMUIA ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imetoa onyo kwa watu wa Burkina Faso kwamba katika vurugu za sasa za kisiasa, haitatambua hatua yoyote ya kutwaa madaraka kwa njia zisizo za kikatiba.
Hayo yamo katika taarifa iliyosainiwa na Rais wa ECOWAS, John Mahama, aliyesema jumuia hiyo “imefuatilia kwa wasiwasi mkubwa matukio nchini Burkina Faso yanayotokana na muswada wa mabadiliko ya katiba.”
Katika vurugu hizo, waandamanji walilichoma bunge la nchi hiyo wakipinga Rais Blaise Compaore, aliyeiongoza nchi hiyo kwa miaka 27, kutaka katiba ifanyiwe mabadiliko ili aweze kugombea tena nafasi hiyo mwaka kesho.
Hata hivyo, bunge la nchi hiyo limesimamisha upigaji kura hiyo ili kumpa Compaore fursa ya kugombea tena. Kiongozi huyo, alitwaa madaraka katika mapinduzi ya mwaka 1987 na akashinda katika chaguzi nne zilizofuata na ambazo matokeo yake yalizua malalamiko.
Mahama alisema ECOWAS imeutambua uamuzi wa serikali wa kuondoa muswada huo, akisema ni hatua yenye lengo la kuendeleza utulivu na amani katika nchi hiyo, na amewataka wananchi wa Burkina Faso kuwa watulivu na kutii sheria, na akayataka majeshi ya usalama kuheshimu katiba ya nchi.

No comments:

Post a Comment