Wednesday, 29 October 2014

BABA TEGETE AIVAA UONGOZI WA YANGA!

 

 Straika wa Yanga, Jerry Tegete.
SIKU chache baada ya straika wa Yanga, Jerry Tegete kuiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi ugenini tangu kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu Bara msimu huu ilipocheza dhidi ya Stand United ya Shinyanga, baba mzazi wa mchezaji huyo, Mzee John Tegete, ameuvaa uongozi wa klabu hiyo na kuutaka uache majungu.
Tegete aliifungia Yanga mabao mawili ilipoitandika Stand United mabao 3-0, Jumamosi iliyopita mjini Shinyanga na kuifanya ipande juu katika msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi kumi.
Nyota huyo ambaye alijiunga na Yanga akitokea Shule ya Sekondari Makongo, hivi sasa ndiye anayeongoza kwa kuzifumania nyavu klabuni hapo pamoja na kwamba amecheza dakika 20 tu.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mzee Tegete alisema kuwa mwanaye huyo amewaziba midomo wale wote waliokuwa wakimchukia na kumfanya akose nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu kuliko mchezaji mwingine klabuni hapo kwa hivi sasa.
Alisema kitendo cha mwanaye huyo kuwa benchi muda mwingi bila ya kucheza kilikuwa kikimuumiza sana na alikuwa akiwapigia kelele mara kwa mara viongozi wa Yanga juu ya jambo hilo, lakini waliziba masikio kwa sababu tu ya chuki binafsi.
“Siku zote nilikuwa nikimwombea mazuri mwanangu juu ya wale wanaomchukia kwa kila nilipokuwa nikiwauliza kwa nini hachezi, waliniambia kuwa hachezi kwa sababu anapokuwa uwanjani hufanya mzaha, jambo ambalo si kweli kabisa, Tegete hayupo hivyo ila yeye ni mtu wa watu na hupenda kucheka na kutaniana na kila mtu.
“Hata hivyo, pamoja na yote hayo, namshukuru Mungu, mwanangu ameonyesha kuwa yeye ni bora zaidi katika kikosi cha Yanga hata kama wanamchukia lakini atabakia kuwa bora,” alisema Mzee Tegete ambaye pia ni kocha mkuu wa timu ya Toto African ya jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment