Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri.
UNAKUMBUKA?
Uongozi wa Simba ulimpa Kocha Mkuu Patrick Phiri mechi mbili
kuhakikisha anapata ushindi vinginevyo kibarua kitaota nyasi lakini
tayari ameshaharibu moja, baada ya kutoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar
juzi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro....
Phiri ambaye hajaonja ladha yoyote ya ushindi kwenye ligi msimu huu
kikosi chake kikiwa kimetoka sare sita, sasa amebakiza mechi moja tu ya
kuhakikisha anasawazisha makosa na mechi yenyewe ni dhidi ya Ruvu
Shooting.
Lakini Ruvu Shooting wakijua kwamba Phiri anatakiwa ashinde mechi
hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili ijayo, wamemwambia
aanze kukusanya virago.
Akizungumza na Championi Jumatatu, msemaji wa Ruvu Shooting, Masau
Bwire, alisema wamejiandaa vya kutosha kuhakikisha wanaibuka na ushindi
katika mchezo huo dhidi ya Simba baada ya kuzikosa pointi tatu katika
mchezo dhidi ya Coastal Union.
“Tunapenda kumwambia Phiri kuwa aanze kujipanga kwa safari ya kurudi
kwao Zambia kwa sababu tumejiandaa vya kutosha kwa ajili ya kuifunga
timu hiyo.
“Mchezo huo utakuwa ndiyo wa mwisho kwa Phiri kutokana na kujipanga
kwetu, ukichanganya na hasira ya kuzikosa pointi tatu katika mchezo wetu
uliopita dhidi ya Coastal,” alisema Bwire.Lakini Phiri mwenyewe amepata
kigugumizi kuhusiana na kuelezea kiufundi kinachoisibu timu yake, kwani
amedai haelewi kinachoendelea.
Phiri amesema wachezaji wake wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri
uwanjani lakini hawapati matokeo mazuri.“Nashangaa kwa nini tunapata
matokeo ya namna hii, kiukweli wachezaji wangu kama leo wamecheza vizuri
sana ingawa wamepoteza nafasi kadhaa, sijui kitu gani kinatokea, kama
ni bao tulianza kufunga sisi, ingawa na wapinzani walikosa penalti,”
alisema Phiri.
Simba ipo katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa
na pointi sita, baada ya kushuka dimbani mara sita. Ruvu yenyewe ipo
nafasi ya saba, ikiwa na pointi saba.
No comments:
Post a Comment