Mbunge wa Kisesa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Luhanga Mpina akizunumza kwenye moja ya vikao vya Bunge mjini Dododma.
WANANCHI wa kada mbalimbali nchini, wamempa ‘big up’
na kumuunga mkono Mbunge wa Kisesa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Luhanga Mpina (pichani) kwa kitendo chake cha kuomba Bunge la Jamhuri ya
Muungano kusitisha mikutano yake, ili fedha zinazolipwa kwa wabunge
ziiwezeshe serikali kulipa deni la shilingi bilioni 90 inazodaiwa na
Bohari Kuu ya Madawa (MSD) iliyogoma kutoa dawa kwa hospitali za umma...
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara tu baada ya Mpina kutoa kauli
hiyo Jumanne wiki hii bungeni Dodoma, wananchi hao wamesema kitendo
hicho ni cha kishujaa na kimeonyesha uzalendo wa hali ya juu bila kujali
itikadi za kisiasa.
“Hii ni aibu kwa serikali, inashindwa kulipa deni kwa muda mrefu hadi
MSD inashindwa kujiendesha, sasa wanapokataa kutoa dawa, maana yake ni
maumivu kwa wananchi wa hali ya chini, hasa wa vijijini. Bora wao wa
mijini wanaweza kwenda kununua kwenye maduka ya dawa. Serikali haijali
kwa sababu vigogo wake wanatibiwa nje kwa hiyo hawaoni umuhimu wa kulipa
deni hilo kwa sababu haliwagusi,” alisema Felix Duni aliyejitambulisha
kama mjasiriamali, mkazi wa Mbagala, Dar.
John John, mwenyeji wa Nzega mkoani Tabora, alisema hakutegemea kama
hoja hiyo ingeweza kutolewa na mbunge wa CCM, kwani kufanya hivyo ni
kama kuivua nguo serikali yake, hivyo ujasiri wake unapaswa kuigwa,
kwani vikao vya bunge havina umuhimu kuliko afya za wananchi
wanaowawakilisha.
“Wao wamechaguliwa na wananchi, katika hali kama hii, lazima waungane
kutetea afya zao, serikali lazima itilie maanani suala hili, Bohari Kuu
ya Madawa inabebeshwa mzigo wa bure, kwa nini deni linakuwa kubwa kiasi
hiki wakati kila mwaka wizara ya afya inapewa pesa? Tunataka wabunge
kama hawa wenye kujali wananchi wao,” alisema John alipozungumza kwa
njia ya simu.
Gazeti hili lilipokea simu pia kutoka kwa wananchi wa Mikoa ya
Singida, Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam, ambao walitoa pongezi nyingi
kwa mbunge huyo na kumtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kulipa uzito
jambo hilo, vinginevyo, waishinikize serikali kulipa deni hilo.
Baada ya mbunge huyo kutoa ombi hilo, Naibu Spika, Job Ndugai
alimjibu kuwa suala hilo litapelekwa kwa Kamati ya Uongozi wa Bunge ili
kujadiliwa na kwamba jibu lake litatolewa. Hadi gazeti hili linakwenda
mtamboni, bado jibu lilikuwa halijatolewa.
Bohari Kuu ya Madawa ilisitisha kutoa huduma kwa baadhi ya hospitali
za serikali kutokana na deni kubwa ambalo halijalipwa kwa muda mrefu.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili peke yake, inadaiwa kiasi cha shilingi
bilioni tisa, kitendo kilichosababisha hospitali hiyo kubwa ya umma
kupandisha ada kwa wagonjwa wanaolala na vitanda, jambo ambalo
limelalamikiwa sana na wananchi.
No comments:
Post a Comment