NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu unaendelea vizuri na kazi ya
kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo kupitia ujasiriamali. Mada
tunayoendelea kuijadili ni sababu zinazofanya watu wengi washindwe
kufanikiwa....
Wiki iliyopita, niliishia kueleza kwamba watu wengi hawafanikiwi kwa
sababu hawawezi kuwa mabahili katika matumizi ya pesa wanazozipata.
Niliishia kukupa mfano wa jinsi mimi na dada yangu tulivyokuwa na hulka
tofauti za matumizi ya pesa tulipokwenda kwenye mashindano ya Umiseta
mjini Songea.
Kabla sijaendelea mbele, ningependa kumalizia mfano huo:
Kabla sijaendelea mbele, ningependa kumalizia mfano huo:
Mzee wetu alitupatia Sh. 5,000 kila mtu kama ‘pocket money’ na pesa
ya kutumia njiani wakati wa safari. Kwa wakati huo ilikuwa ni pesa
nyingi sana kwa mwanafunzi. Pengine kwa nyakati hizi ingekuwa ni zaidi
ya shilingi laki moja.
Cha kushangaza ni kwamba, mara baada ya kufika tu Songea ambako
tulipaswa kukaa kwa wiki moja kamili mimi nilianza kutumia ile pesa
hovyohovyo kama vile kununua chips kuku, soda za mara kwa mara pamoja
na marafiki, kwenda muziki n.k.
Baada ya siku mbili tu, nikawa nimeishiwa kabisa. Sasa kumbuka mwaka
1992 shilingi 5000 ni pesa nyingi sana. Baada ya hapo nikawa sina ujanja
zaidi ya kwenda kucheki na dada Mary kama yeye alikuwa bado na kiasi
ili anikopeshe.
Kilichonishangaza ni kwamba Mary alikuwa hajatumia hata senti moja
katika ile 5000/- yake! Wow! Hilo jambo lilinishangaza kupita maelezo ya
kawaida. Hivyo ilikuwa wazi kwamba mimi nilikuwa mfujaji wakati dada
yangu alikuwa mtunzaji. Je, wewe ni mfujaji au mtunzaji?
Wakati mwingine ambapo somo hili lilijirudia vizuri sana, ilikuja
kuwa takriban miaka 13 baadaye. Mwaka 2005 nikiwa kwenye ajira zangu za
mwisho mwisho kabla sijajiajiri, nilikuwa nafanya kazi kama ofisa mauzo
wa Apsi Business Manager jijini Dar es Salaam. Kampuni ilikuwa ndogo ya
wastani yenye watu kama 10 hivi pamoja na wakurugenzi wake.
Lakini kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa mesenja pale ofisini kwa
jina la Jose. Mara kwa mara, baada ya sisi sote wafanyakazi (kasoro
wakurugenzi kuishiwa) tulikuwa tunakimbilia kwa Jose kumuazima pesa.
Pamoja na kwamba Jose alikuwa na mshahara mdogo kuliko wote, lakini
ndiye aliyekuwa na udhibiti mkubwa wa pesa kuliko sisi maofisa wengine
wote! Ni ajabu sana.
Hivyo, haijalishi unalipwa kiasi gani cha pesa kila siku, wiki au
mwezi, inajalisha unaweza kutunza kiasi gani cha pesa hiyo. Kwa hivyo
weka malengo ya kudhibiti pesa yako leo ili uanze kuchangisha kwa ajili
ya mtaji wako wa biashara au kwa ajili ya mambo ya msingi zaidi
maishani.
No comments:
Post a Comment