Tuesday, 11 November 2014

KASHFA MENO YA TEMBO NA MAJIBU MEPESI YA SERIKALI.

KASHFA iliyoibuliwa na Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira ya Uingereza, (Environmental Investigation Agency kwa kifupi EIA), dhidi ya serikali kuhusu ziara ya Rais wa China, Xi Jinping hapa nchini kuwa msafara wake uliondoka na shehena ya meno  ya tembo ni nzito inayolitia doa taifa....

Kwa uzito wake, nafsi yangu kama mzalendo na muumini wa  heshima kwa viongozi wangu na taifa langu nilitaraji majibu ya serikali yangeendana na ukubwa wa kashfa hiyo inayolidhalilisha taifa letu.
Kwangu mimi, naona siyo sawa kuituhumu ripoti ya EIA na kuiita ni ya kupikwa bila kuonesha kinagaubaga kupikwa huko ni kwa namna gani na kumetokana na nini?
Kama hilo halitoshi, siyo sahihi pia kuishia kwenye kikomo cha uongo wa taarifa bila kuvitaka vyombo husika vilivyoripoti habari hiyo vieleze ukweli wa jambo hilo, kwa kuwa ni wazi sheria za vyombo vya habari duniani zinakataza kutangaza taarifa ya uongo.
Nasema hivyo kwa sababu maudhui ya habari iliyotangazwa ni mapana zaidi. Lingekuwa jambo la kawaida kama mkono wa taarifa hiyo ungekuwa unawahusisha watu fulani kwa aina ya uraia wao lakini siyo taasisi nyeti za nchi kama ikulu.
Ni jambo zito na la fedhaha kubwa kuutangazia ulimwengu kuwa msafara wa rais wa China ambao kiprotokali ulipokelewa na kusindikizwa na rais wa Tanzania na maofisa wa ngazi za juu wa usalama kuwa ulihusika na uhujumu uchumi, halafu majibu ya serikali yakaishia kwenye kauli za kusema habari hiyo ni ya uongo na wivu tu bila kuvuka mpaka huo.
Kama mzalendo, majibu hayo hayajaniondolea aibu kwa nchi yangu; hayajamrudishia heshima rais wangu na yameshindwa kurejesha heshima ya Watanzania kimataifa kwa sababu ni mepesi mno!
Ninaposema mepesi nina maanisha kwamba, majibu hayo yana maswali ndani yake; hayamalizi mjadala na hayamtaji mkweli ni nani kati ya EIA, vyombo vikubwa vya habari vya nje na serikali.
Kama tunaweza kuwa na taasisi, vyombo vya habari vinavyoweza kuingilia uhuru wa nchi yetu kwa kiwango hicho na kuviacha bila kuvichukulia hatua zinazoshtahili, kama taifa tunawezaje kujenga heshima?
Katika sakata hili bado kuna mambo mawili ya kuamini kutokana na mazingira yalivyo; Kwanza ni kuwepo kwa ukweli wa tuhuma za uhujumu uchumi zinazolihusisha taifa kubwa kinara wa soko la meno ya tembo duniani kwa kushirikiana na watawala wetu kujihusisha na biashara haramu.
Pili ni kupikwa kwa skendo hiyo kwa malengo yasiyojulikana kama majibu ya serikali yalivyodai na hivyo kulifanya taifa lionekane sawa na simba wa chuma ambaye hata watoto wanaweza kumchezea watakavyo.
Kwa mtazamo; mambo yote mawili ni ya aibu! Ikiwa ni kweli viongozi wetu wamefika mahali pa kushirikiana na wahujumu uchumi kufanya hata biashara haramu ujue kaburi la maendeleo ya taifa limeshachimbwa na muda mfupi ujao nchi itazikwa na aibu itakuwa juu ya viongozi wa awamu hii.
Aidha, kama jambo hili haliko hivyo na kwamba kuna wahuni wamepika taarifa hizo kwa lengo la kufanikisha matakwa yao, bado pia ni jambo la aibu kama serikali ya China na Tanzania zitakubali kufanyiwa uzushi mkubwa kiasi cha kuihusisha hadi ndege ya rais kubeba mali za magendo, huku maofisa wa usalama wakitajwa kuhusika moja kwa moja na biashara haramu.
Kwa mtazamo huu, kama serikali inaziamini kauli zake juu ya kashfa hii nzito kuwa habari ni za uongo njia pekee ya kuufuta uongo huo ni moja; nayo ni ya kuujulisha ulimwengu  kwa vielelezo kuwa taarifa hizo siyo sahihi kwa kuweka ushahidi mezani.
Ikishindwa kufanya hivyo itajikuta imeangukia katika kipengele kimoja wapo kati ya nilivyovitaja; cha kuhusika ambacho ubaya wake ni watawala wa nchi kujihusisha na ufisadi au kutohusika ambako kutawaweka pia viongozi wa nchi katika fungu la watu dhaifu wanaoweza kuzushiwa vitu vibaya kama hivyo wakanyamaza.
Nashauri; hatua zaidi ya kauli za serikali zichukuliwe ili kuiondoa kashfa hii. Kwanza utangazwe mgogoro na taasisi ya EIA juu ya taarifa zake, kushinikiza iwasilishe kwenye vyombo vya kimataifa ushahidi wa taarifa hiyo na ikishindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zichukuliwe sambamba na vyombo vya habari vilivyoripoti habari za uongo dhidi ya serikali ya Tanzania, vinginevyo, hatuweza kujivika nguo kwa maneno bali vitendo.

No comments:

Post a Comment