Naendelea kuwaletea maelezo kuhusu maisha ya Askofu Kakobe baada ya
kuokoka na kuanzisha kanisa.Mwandishi: Kuna waliosema kuwa ulianzisha
kanisa nchini Marekani na ulikuwa na mpango wa kuhamia huko, je ni
kweli?..
Askofu Kakobe.
Askofu Kakobe: Kuhama nchi siwezi lakini ni kweli baada ya maombi ya
muda mrefu Aprili 16, 2012 nilifungua kanisa Marekani, hii ni nia ileile
ya kuokoa mataifa na kuinua jina la Yesu.
Mwandishi: Tunaona watu wakifunga ndoa wanavaa pete lakini katika kanisa lako hilo halipo, unazungumziaje hilo?
Askofi Kakobe: Pete kwenye ndoa siyo agizo la Bwana na ndiyo maana
tunaona Mungu mwenyewe akichukizwa na watu waliovaa pete, vikuku na
mapambo mengineyo. Soma maandiko haya Isaya 3:21, 16-24; Hosea 2:13;
Mwanzo35:1-5; Kutoka 33:4-6; Yeremia 4:30; 1Timotheo 2:9-10; 1Petro
3:3-5. Mapambo ni mavazi ya waabudu miungu, yanahusishwa na ibada ya
miungu (mashetani).
Mwandishi: Lakini wanaotumia pete katika ndoa wanasema eti pete ni
mfano wa upendo usio na mwanzo na mwisho, unasemaje kuhusu madai hayo?
Askofu Kakobe: Hiyo siyo kweli, mwanzo wa upendo ni pale walipokutana
na wakapendana na mwisho wa upendo ni pale mmoja anapofariki na
kumfanya mwenzake kuwa huru kuolewa au kuoa. Yesu alisema mbinguni
hakuna kuoa wala kuolewa.
Hutapewa mke wako au mume wako uishi naye huko mbinguni. Yote hii ni
janjajanja ya shetani anayekuja kwa mfano wa malaika wa nuru ili
kutufanya tuingize mapambo katika nyumba ya Mungu na kujenga ngome za
mashetani kwa visingizio kwamba mimi nimevaa pete sasa ni mke wa mtu au
mume wa mtu. Mbona nyumba za wageni (guest houses) zimejaa watu wenye
pete za ndoa? Kama pete hizo zingekuwa zinawafanya watu wasiwe makahaba,
tusingekuwa na matatizo tuliyonayo leo.
Mwandishi: Umekuwa ukihubiri wokovu, nini maana ya neno kuokoka au kuokolewa kidini?
...Akiwa kwenye moja ya mahubili yake.
Askofu Kakobe: Kuokoka au kuokolewa ni kunusurishwa, kuopolewa,
kusalimishwa au kuponywa kutoka katika maafa makubwa yaliyo dhahiri
kabisa kukupata. Inaweza ikawa kuponywa kutoka katika hatari ya kifo,
adhabu kali au madhara yoyote makubwa yaliyo dhahiri.
Katika hali ya kukosa matumaini ya kukwepa maafa hayo yaliyo dhahiri,
inapotokea ghafla njia ya kusalimika, hapo inasemekana umeokoka. Mtu
mwenye dhambi ni lazima atapata adhabu ya milele. Adhabu yake inaitwa
mauti ya pili au mauti ya milele ambayo ni kutupwa motoni na kuteswa
milele. Hakuna mwenye dhambi atakayekwepa adhabu. Kila mmoja atapata
mshahara huo wa dhambi, mauti ya milele au kutupwa Jehenamu ya moto.
Mwandishi: Unawashuri nini wasomaji wanaokusoma sasa katika safu hii kuhusu hilo?
Askofu Kakobe: Nawashauri kwamba njia rahisi kuepuka hayo ni kuokoka.
Huwezi kuacha dhambi kwa nguvu zako au uwezo wako! Dhambi ina nguvu na
uwezo juu ya mwanadamu. Kwa nguvu zako, utajaribu kuacha sigara na
kutafuna pipi au peremende lakini siku mbili tatu unajikuta unarudia
tena kuvuta sigara. Kiu ya sigara huwezi kuishinda kwa uwezo wako.
Kwa nguvu zako utajaribu kuacha uasherati na uzinzi kwa kuogopa
magonjwa ya hatari kama Ukimwi, kisonono au kaswende; lakini utajikuta
baada ya muda mfupi tamaa iko palepale. Utajitahidi kuacha pombe lakini
muda mfupi unashindwa kabisa kuishi bila kunywa pombe. Ni lazima ukiri
kwamba huwezi. Dini haiwezi kumfanya mtu aishinde dhambi.
Tangu uwe na dini, hujaweza kushinda dhambi. Watu wenye dini ndiyo
ambao wamejaa magerezani wakiwa ni wahalifu wakubwa. Unachotakiwa
kufanya ni kusalimu amri na kuanguka miguuni pa Yesu Kristo aliyeshinda
dhambi, yeye atakupa msaada na uwezo wa kuishinda dhambi.
Mwandishi: Wapo watu wanasema Yesu alibadili divai na kuwa pombe lakini pombe inakatazwa katika dini, unaweza kufafanua hilo?
Askofu Kakobe: Muujiza wa kubadili maji kuwa divai kwa Yesu, ulikuwa
mkubwa. Nzio moja ni karibu na galoni 9. Nzio tatu ni galoni 27.
Mabalasi sita yalikuwa na ujazo wa nzio kama 18 au galoni 18 mara 9 au
27 mara 6 ambayo ni sawa na galoni 162 au debe 40½ ambazo ni karibu
mapipa saba.
Itaendelea wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment