Tuesday, 28 October 2014

"KAMA SIO MGUU NINGEKUA CHUO KIKUU" NDIVYO ANAVYOSEMA KIJANA HUYU


Kijana Sweetbart Joseph (22), mkazi wa  Mbezi Salasala jijini Dar es Salaam, analia na kuhangaika huku akiwa kitandani kwa miaka nane sasa kutokana na mguu wake wa kushoto kuwa na uvimbe mkubwa unaomfanya ashindwe kutembea.

 
Kijana Sweetbart Joseph (22) anayesumbuliwa na matatizo ya uvimbe mguuni.
CHANZO CHA TATIZO
Akizungumza na waandishi wa habari hii nyumbani kwao Mbezi Salasala,  Sweetbart alikuwa na haya ya kusema:“Nilianza kuteseka tangu mwaka 2005, nikiwa darasa la sita ambapo mguu wangu ulianza kuvimba kidogokidogo mpaka nikawa nashindwa kuvaa kiatu. Ilibidi kiatu cha mguu huo nikipeleke kwa fundi ili kukiongezea ukubwa.
“Nilimaliza elimu ya msingi kwa shida na nilipojiunga na kidato cha kwanza nilisoma kwa shida kutokana na kusumbuliwa na mguu huu ambao umevimba. “Kuna kipindi nilipata homa kali kutokana na kusumbuliwa na mguu huu ambao ulikuwa ukinifanya nione kama ni jipu kubwa na kusababisha niwe nakwenda Hospitali ya Temeke kutibiwa.
AFANYIWA UPASUAJI USAHA LITA TATU WATOKA
“Siku ya kwanza nilipokwenda Hospitali ya Temeke waliamua kunipasua wakatoa lita tatu za usaha. Walinisafisha kisha wakaniruhusu nirudi nyumbani.
 
Muonekano wa karibu wa mguu wa Sweetbart uliovimba.
“Nikiwa nyumbani nilipata nafuu, lakini sikuweza kukaa muda mrefu mguu ukaanza kuuma. Maumivu niliyopata nashindwa namna ya kuyaelezea, nikawa mtu wa kulia tu!
Kutokana na hali hiyo nikawa nakosa usingizi, wenzangu wakiwa wamelala mimi nikawa nakesha macho.
“Hali yangu ilipozidi kuwa mbaya nilipelekwa tena Hospitali ya Temeke, daktari mmoja aliamua  nilazwe kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kubaini kilichosababisha mguu wangu kuvimba,” alisema kijana huyo.
Akiendelea kuzungumza alisema kuwa kutokana na mguu wake huo kumsumbua hata kusoma alikuwa anasoma kwa shida sana japokuwa alikuwa na uwezo kimasomo darasani.“Ilibidi baadaye nikae tu nyumbani huku nikiugua mguu ndipo wazee wangu wakaamua kubadili sehemu ya kutibiwa, kama siyo mguu huu nina hakika ningekuwa nasoma chuo kikuu,” alifafanua kijana huyo huku akionekana mwenye huzuni.
KUHAMIA MUHIMBILI
“Nilikwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako walinipokea na kunifanyia vipimo vyote hadi vya kansa na mwisho walinishauri nikatibiwe nje ya nchi.“Baada ya kuambiwa natakiwa kwenda kutibiwa nje, kuna mtu mmoja alimtafuta daktari wa nchini India akamweleza tatizo langu akamwambia anaweza kunitibu na kupona kwa gharama ya shilingi milioni sita.
 
Sweetbart akitafakari jambo.
NALIA KILA SIKU
“Baada ya kuambiwa gharama hiyo nililia sana kwani familia yangu haina uwezo huo, nikajua kilicho mbele yangu ni kifo kwa sababu ya kukosa kiasi hicho cha fedha ili nikatibiwe nchini India,” alisema kijana huyo huku akifuta machozi yaliyokuwa yakimtiririka.
Ilibidi waandishi wetu wakae kwa dakika kadhaa huku wakimpa pole kwa tatizo alilokuwa nalo, baada ya kupangusa machozi akaendelea kusema:“Nalia kwa sababu maisha yangu ni duni na wazee wangu hawana uwezo wa kunipeleka kutibiwa nje ya nchi kwa gharama ya shilingi milioni sita nilizoambiwa.
“Kutokana na kushindwa huko, naendelea kuteseka huku nikiwa kitandani, sijui nitaponaje maradhi haya ambayo yananitesa mwaka wa nane sasa.Naamini kama nisingekuwa naumwa hivi sasa ningekuwa na hatua kubwa kimasomo na mambo mengine lakini ndiyo hivyo, nimekuwa mtu wa kulala ndani tu huku nikipata maumivu makali kila kukicha.

KILIO KWA WATANZANIA
“Nawaomba Watanzania wenzangu waliosoma habari yangu wanisaidie chochote walichonacho kwani naamini kama nitapata fedha hizo na kwenda kutibiwa India nitapona na kuwa mtu mwenye furaha na amani kama wengine.
“Yeyote aliyeguswa na mateso yangu anaweza kunisaidia chochote atakachobarikiwa kwa kutumia namba 0713 739253, ” alisema Sweetbart.
Bila shaka baada ya kusoma habari hii ya kijana Sweetbart umegundua ni kwa kiasi gani anahitaji msaada wako wa hali na mali, kama umeguswa na unapenda kumsaidia tumia namba yake iliyopo hapo juu.Shime Watanzania, kutoa ni moyo na siyo utajiri na Mungu atakupa baraka zake- Mhariri.

No comments:

Post a Comment